Jumatano 11 Juni 2025 - 20:16
Haramu Tukufu ya Alawi yatangaza ratiba yake ya awamu ya kumi na nne ya wiki ya kimataifa ya Ghadir

Hawza/ Haramu tukufu ya Alawi imetoa maelezo kamili kuhudiana na kuanza shughuli za kila mwaka za wiki ya kimataifa ya Ghadir.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya  Shirika la Habari la Hawza, Haramu Tukufu ya Alawi imetoa maelezo kamili kuhusiana na kuanza kwa shughuli za kila mwaka za wiki ya kimataifa ya Ghadir, Shughuli hizi, katika awamu yake ya kumi na nne, zitafanyika ndani ya kumbi za haramu ya Am'irl-M'umina (as), katika mfumo wa ratiba ya kidini, kiutamaduni na kisanaa, ambayo ni ya kwanza na ya aina yake katika hafla na sherehe za kumbukumbu zinazofanyika ndani na nje ya Iraq.

Taarifa hii imetangazwa kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na Haidar Rahim, Mkuu wa Idara ya Habari ya Haramu Tukufu ya Alawi, katika eneo la bi Zainab (sa) lililoko kwenye ukumbi wa bi Amina (sa). Kwenye mkutano huo walihudhuria waandishi wa habari kutoka vituo vya setalaiti, mashirika ya habari, pamoja na kundi la waandishi wa habari wa magazeti, wataalamu wa vyombo vya habari na watayarishaji wa maudhui.

Akaongeza kuwa: “Shughuli za wiki ya kumi na nne ya kimataifa ya Ghadir zilianza mapema wiki hii kwa kutangazwa rasmi na kusherehekewa kwa kiwango cha ndani, kitaifa na kimataifa. Jumla ya shughuli 40 zimepangwa kufanyika ndani ya kipindi cha wiki moja, ambapo ni kilele cha jitihada za idara mbalimbali zinazofanya kazi ndani ya haramu kwa uratibu na "Kituo cha Mipango na Maendeleo ya Nidhamu", kwa ajili ya kuangazia tukio hili lenye harufu ya utukufu kama njia ya kuunganisha fikra ya Ghadir na uhalisia wa kijamii na kiutamaduni wa zama zetu, kupitia ratiba ambazo zinadhihirisha utambulisho wa Imam Ali (as) kama mfano wa uadilifu, elimu na ubinadamu.”

Haidar Rahim alitaja miongoni mwa shughuli kuu za Wiki ya Ghadir kuwa ni kupandishwa kwa bendera tukufu ya Ghadir ndani ya haramu ya Am'iril-M'uminina (as), katika mikoa mbalimbali ya Iraq na mabara mbalimbali duniani, ambapo zaidi ya bendera 700 zitapandishwa ambapo baadhi ya hizo zikiwa katika hafla rasmi na za kipekee.

Akaendelea kusema kuwa: bendera nyingine zitapandishwa katika sehemu za kijamii, kidini na kiutamaduni ndani ya Iraq na duniani kote, katika mabara yote ya Asia, Afrika, Ulaya, Amerika na Australia, katika nchi 40, ukiachilia mbali, mita takriban 35,000 zitapambwa katika mji mtakatifu wa Najaf Ashraf na maeneo ya viunga vyake.

Rahim aligusia pia hatua ya Haramu Tukufu ya Alawi kuanzisha mradi wa kipekee kwa jina la “Kumbukumbu ya Ghadir”, ambao utakuwa katikati ya mji wa Najaf Ashraf. Mnara huu utakuwa ni jengo la usanifu wa kisasa lenye hadhi ya kihistoria na kivutio cha utalii na huduma, lenye eneo la zaidi ya mita za mraba 50,000, na utakuwa ukijumuisha tukio la milele la Ghadir kwa mtindo wa usanifu wa kisasa unaodhihirisha asili na kugusa dhamira. Huu ndio mnara wa kwanza wa kudumu wa aina yake kuasisiwa katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kumbukumbu hiyo.

Mkuu wa Idara ya Habari alieleza pia kuwa kutafanyika kongamano la kielimu kuhusu sikukuu ya Ghadir litakaloshirikisha watafiti kutoka nchi 10, pamoja na kuonyeshwa tamthilia katika sehemu ya mapumziko ya al-Nakheel yenye ukubwa wa mita za mraba 10, itakayoweza kuwapokea zaidi ya watu 6,000. Pia, kutakuwa na maonyesho ya nakala adimu na za kihistoria za Qur’ani Tukufu zitakazoonyeshwa kwa mara ya kwanza, pamoja na maonyesho ya kisanii na kuta za kuchora michoro ya sanaa.

Aliongeza kuwa: shughuli hizi zitahusisha pia ratiba maalumu kwa ajili ya watoto, maandamano ya watu wanaowapenda Ahlulbayt kwa ajili ya mayatima, pamoja na kuzinduliwa kwa tovuti maalum na shindano la kielektroniki.

Mkuu wa Idara ya Habari ya Haramu ya Alawi alisisitiza juu ya kuandaliwa kwa jukwaa la habari na kituo cha habari kilichounganishwa kikamilifu ambacho kitajumuisha mahitaji yote ya wataalamu wa habari, sambamba na kutumwa kwa ujumbe wa pongezi milioni tano kwa njia ya SMS kwa ajili ya kusherehekea tukio hili tukufu.

Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Haramu ya Am'iril-M'uminina Ali (as) alihitimisha hotuba yake kwa kutangaza maandalizi ya maeneo kwa ajili ya kuwakaribisha mahujaji wa sikukuu ya Ghadir na wiki hiyo tukufu kupitia maeneo 10 makuu na mawakibu 15 ya wananchi yatakayoungwa mkono na haramu tukufu kwenye huduma na ufadhili. Aidha, eneo la kudumia la ukarimu limeandaliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Najaf Ashraf kwa ajili ya wageni kutoka nje ya Iraq wanaokuja kwa ajili ya kushiriki katika tukio hili adhimu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha